Mahubiri na Shuhuda
Get Adobe Flash player

Somo la Maombi

Utangulizi.

Awali ya yote,ninakusalimu sana katika jina la Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo aliyekufa msalabani na kufufuka  kwa ajili yetu ili kutuokoa toka  dhambini. Lakini pia nikukaribishe  kupitia katika tuvoti yetu ya www.mgmtministry.org, kisha utaendelea kutufuatilia kwenye mitandao wa twitter,face book, Linklin na Youtube.

Shukrani.

Nianze kwa kumshukuru sana Mungu kwa kuniwezesha kuanza kufundisha masomo yangu kupitia katika tuvoti yetu ya  The  Ministry of God’s Message Tanzania(MGMT) kuanzia sasa na siku zijazo ikiwa Bwana ataendelea kutulinda. Ninayo masomo mengi ya kufundisha Mungu akitupa neema zaidi, ingawa si kwa undani sana ila katika kila mwisho wa somo tutakuwa na kuchangia kwa kutoa maoni na kuuliza maswali. Tumeweka nafasi hiyo kwa makusudi kabisa ili kukusaidia kuyajibu maswali yako ikiwa utayapata baada ya kujifunza somo.Tafadhali itumie kwa faida yako mwenyewe na wengineo. Masomo haya yanawafaa watu wote watakaopenda kujifunza neno la Mungu kupitia kwenye tuvoti yetu, mitandao ya twitter,na face book, na Linklin kama nilivyokwisha sema. Pamoja na masomo mengi tutakayo jifunza, kwa sasa tutaanza na somo la maombi.

Kila dini hufundisha kuomba.

Nimeaanza na somo hili kwa sababu dini zote zilizoko duniani  zinafundisha namna ya kuomba, ingawa baadhi ya waumini wa dini nyingi  hawajui kwa hakika wanamwomba nani  au Mungu yupi, ila wanaamini na kufundishwa   kumwomba  Mungu ambaye anasikia sala zao kama wanavyofundishwa na viongozi wao wa dini. Bado waumini  wengi hawajui  huyo Mungu wamwombaye  yuko wapi na anafanya nini hasa. Kwa mfano, wako watu wanaokwenda makaburini kuomba kwa kuitambikia mizimu ili  itatue matatizo yao,hali wengine wakiomba wafu wawasaidie kutatua matatizo yaliyozikumba familia zao,n.k.  huku baadhi yao wakiamini kabisa kwamba huyo mungu au mizimu waiombayo  inasikia maombi yao na “kuyajibu” ingawa hawana  uhakika watajibiwa lini au  kwa njia gani na kwa vipi.

Maombi ya kanisa.

Kwa upande wa kanisa, tutajifunza na kuona jinsi  ambavyo baadhi ya  waalimu walivyofundisha  somo la maombi kwa kutumia  “staili” mbalimbali kama tutakavyojifunza.Hata hivyo,vitabu vingi vimeandikwa vihusuyo maombi lakini kila mtu ameandika kufuatana na ufunuo wake  kwa   jinsi Mungu alivyomfunulia,hivyo mafundisho yanatofautiana. Kwa bahati mbaya sana, siku hizi somo  la maombi limefundishwa kwa namna tofauti kabisa na Biblia isemavyo,jambo ambalo limeleta wasiwasi na mashaka mengi mioyoni mwa watu. Kwa mfano,baadhi ya waalimu wamefundisha  kwa mkazo wa misingi ya kidini zaidi(madhehebu) bila kusimamia neno la Mungu,hali wengine wakifundisha kwa masilahi binafsi  kiasi cha kuanza “kuyauza” na watu “huyanunua” kutokana na uhitaji wao sawa na mtu anayekwenda kwa mganga wa kienyeji kuaguliwa na kutozwa fedha. Kwa mfano siku hizi yako maombi yanayoitwa ya “express”, maana yake ni kwamba  mtu huaminishwa kwamba akiomba kwa kutumia maombi haya  hufika haraka sana kwa “mungu”  na kujibiwa “haraka”.Baada ya kufanyiwa maombi ya namna hii,“mteja” hupangiwa kiwango cha kutoa “sadaka” kwa kiwango atakachotajiwa   ili “kuyasindikiza” maombi yake! Baadaye hutolewa “unabii”  kwamba atapokea majibu kwa muda mfupi ujao, labda baada ya siku 1,2,3 au wiki kutokana na “dau”  au “uzito” wa sadaka aliyoitoa.

Yako maombi ya “aina” nyingin yanayoitwa ya “kufunguliwa” au “delivarance” kwa Kiingereza. Maombi haya nayo hufanyiwa(huombewa) mtu ambaye ana matatizo yanayodaiwa na “mtumishi” anayemwombea  kwamba  matatizo yake yametokana  au yamesababishwa na  laana, hivyo laani hiyo  inatakiwa “kuvunjwa” kwa maombi ya aina ya “deliverance”. Baada ya mtu kufanyiwa maombi ya “aina” hii, hutakiwa kutoa sadaka “maalum” kwa kuwa  maombi haya huonekana kuwa hujulikana kuwa maombi ya “deliverance” ni “maalum”. Malipo yake huwa ni kuanzia  shs elfu 50- laki 5 kwa kisingizio kuwa ni  “sadaka” kwa Bwana na ule “umaalum” wake.

Mchanganyo wa maombi na vitu mbalimbali.

Yako maombi mengine ambayo watu wamefundishwa kuomba kwa kuchanganya na mafuta ambayo wanadai kuwa ni mafuta ya mizeituni   yaliyotoka nchini “Israeli”.Baada ya mimi mwenyewe kufanya uchunguzi wa kina,niligundua kuwa si kweli kwamba ni  mafuta ya mizeiruni bali ni mafuta ya elizeti na karanga. Huuzwa kuanzia shs  elfu 50 kwa chupa ndogo mpaka laki tatu. Wengine wameaminishwa kutumia kinywaji cha “juice” kwa jina la “fruto” yenye rangi nyekundu ikifananishwa na “damu ya Yesu”ambayo watu  huaminiswa kwamba  mtu anakitumia “fruto” hiyo,mara moja     hugeuka kuwa na nguvu sawa na damu ya Yesu.Huagizwa  waitumie kwa  “kuimwagamwaga” chumbani au sebuleni wakati maombi yakifanyika kwa kusema maneno sawa na mtu “anayewanga” na kusababisha uchafu usio na sababu.

Baada ya kuaminishwa,baadhi ya waumini wamefikia hatua ya kununua katoni nzima ya “fruto”na kuiweka chumbani ili kila tatizo linapotokea,aende kuichukua na kuitumia  kama njia ya kupambana na nguvu za giza. Wako  waumini waliominishwa kutumia chumvi wakati wa kuomba  wakiaminishwa kuwa akitumia hiyo chumvi atakuwa na nguvu ya “ziada” za kiroho ili kuyashinda mapepo au magonjwa ingawa  Biblia inasema  wazi kwamba sisi ni chumvi ya dunia, chumvi ikishaharibika hutupwa nje haifai hukanyangwa na watu Mt 5:12.Maana yake ni kwamba  maisha ya mkristo  yenye ushuhuda mzuri  yamefananishwa na chumvi ambayo ukiweka kwenye chakula huleta ladha nzuri. Mkristo  huyu “akiharibika” kwenye maisha yake yakakosa ushuhuda, huwa hayafai  tena kuwa “chumvi” kwani Yesu atatukanwa badala ya kusifiwa na kutukuzwa.  Maana yake ni kwamba mkristo  akiharibika akakosa ushuhuda  katika maisha yake, hata kama  atatembea na “gunia la chumvi”ili kutumia kwenye “maombi” ni bure kabisa.Chumvi ilitumika katika agano la kale kwa mambo fulani maalum lakini damu ya Yesu ni bora zaidi kuliko chumvi.Kwa wakati huu chumvi inatumika kwa ajili ya miili yetu na si kwa roho zetu. Nimeona na kushuhudia mara nyingi  watu wengi wakiombewa, wakiambiwa watoe sadaka na “kuinenea maneno” wakati  wanapotoa ili ikafanye kazi “iliokusudiwa”. Yako maombi mengine ya kutumia vitambaa ambavyo hudaiwa kuwa “vimeombewa na vina upako”wa ajabu sana  katika kuleta uponyaji na kuondoa shida. Watu wamenunua vitambaa hivyo na kuviweka ndani ili wavitumie wakati wana matatizo au magonjwa. Vitambaa hivi vimeuzwa kuanzia shs elfu 10-100,000!.

Nimeona siku moja nilipokuwa nilifanya huduma ya kumwombea mgonjwa mahali fulani maji yakiwa na picha ya mhubiri mmoja maarufu toka Nigeria kwa maelekezo kwamba mtu akiombewa kwa kutumia hayo maji, atapata uponyaji bila shaka.Pembeni yake kulikuwa na juice aina ya “fruto”. Mgonjwa huyu alikuwa amekata tamaa maana  ametumia vyote  hivi lakini hakuwa amepata uponyaji kwa ugonjwa uliompata zaidi ya miaka mitatu. Nilichofanya nilimweleza juu ya uweza wa damu ya Yesu na kumwamini yeye ili kwamba hata kama hakupona baada ya kuombewa, afe akiwa mikononi mwa Yesu. Waalimu wa uwongo  wako wengi siku hizi wanaofundisha bila kusimamia neno la Mungu, badala yake huandaa maombi katika mazingira ya kutafutia fedha, matokeo yake “watumishi” wengine  wamekuwa “matajiri” kwa kuwaibia watu fedha kwa njia ya maombi ya ajabu kabisa. Hii ni laana kwao.

Pamoja na watu wengi kuombewa na kutoa fedha nyingi ili kupokea “uponyaji” lakini matatizo yako palepale, tena  wakati  mwingine yameongezeka zaidi. Nakumbuka yuko dada mmoja alikuwa mgonjwa akaenda kufanyiwa maombi na “watumishi” fulani jijini Arusha. Alipofika,akaagizwa kununua mafuta ya “ mizeituni” kwa shs elfu 50 waliokuwa nayo wao   wenyewe ,kisha  akapakwa na kutangaziwa uponyaji. Baada ya muda  wa wiki mbili hivi, yule dada akaanza kubakwa  na pepo wakati wa usiku. Ilibidi aanze tena kutafua “watumishi” wengine ili wamsaidie kwa kumwombea. Ilitokea kukutana nami katika moja ya huduma akanieleza kwa kina mkasa wake,nikagundua kuwa “alitapeliwa” kwa njia ya maombi “feki”, lakini  baada ya kumfanyia maombi ya “kawaida” yasiyo na masharti yenye nguvu ya Yesu ndani yake, mapepo yalitimka ndani yake yakisema kwamba yaliingia kupitia kwa “watumishi” aliowafuata kupitia kwenye mafuta ya “mizeituni” aliyonunua yeye mwenyewe na kupakwa. Hizi ni iku za mwisho, ni wakati wa kujihadhari sana na mafundisho yanayofundishwa na waalimu mbalimbali tusiyaamini bila kuyapima kupitia katika neno la Mungu. Tusiziamini kila roho bali tuzipime kama zinatokana na Mungu  mana utapeli ni mwingi siku hizi 1 Yoh 4: 1-3.

Msomaji wangu, nia ya kujifunza somo hili kupitia kwenye tuvoti  yetu ya MGMT, ni katika haya yafuatayo:

  1. Ili kukufundisha na uweze  ukawafundishe wengine walijue somo la maombi wasitapeliwe.
  2.  Ili kila  mwombaji aweze kujitegemea mwenyewe badala ya “kuombewa” kila siku na watu asiowafahamu maisha yao  ya kiroho pamoja na kwamba  wengine wamejiita  ni “watumishi” wa Mungu.
  3. Baada ya kujifunza, somo hili  mtu yeyote “hatanunua”  kama bidhaa adimu madukani, badala yake wataombewa bure bila kutoa malipo yeyote.
  4. Utaona tofauti ya  mafundisho yaliyojegwa kwenye msingi wa agano la kale lililojaa sheria  (analog) na kuingia kwenye mafundisho ya agano jipya, agano la neema(digital).
  5. Mtu atajua hakika kwamba anamwomba Mungu gani (maana iko miungu mingi) badala ya kuaminishwa tu kwamba aombe,na kwamba atajibiwaje maombi yake.
  6. Kupitia kwenye somo hili ambalo pia ninaandika kitabu chake  kinachoitwa Shule ya Maombi  utapata kujua mambo machache lakini muhimu kabla ya kitabu kutoka.Naamini  kitakuwa tayari hivi karibuni, niombee ili nipate fedha za kukidhi gharama za uchapishaji.

Hivyo Roho Mtakatifu akuwezeshe kujifunza  somo la maombi kupitia  katika mafundisho haya  kwa njia ya  facebook, twitter, tuvoti yetu na pia kwenye mtandao wa Youtube. Karibu sana tuendelee kujifunza.

Katika somo hili tutasimamia andiko la neno la Mungu toka Yoh 15:7Ninyi mkikaa ndani yangu na maneno  yangu yakikaa ndani yenu, ombeni  mtakalo lote  nanyi mtatendewa. Kwa mtari huu twaweza kujua na kujifunza kanuni ya maombi, kuwa ni Yesu kukaa ndani yako na wewe kuwa ndani yake, ndipo, uombe lolote naye atakutendea.Tutajifunza mambo yafuatayo:

 

1.Nini maana ya maombi

2.Kazi kuu nne za maombi

3.Vizuizi vya maombi

4.Aina za maombi

5.Majibu makuu manne ya maombi

6.Umuhimu wa kuiombea siku yako ya kufa

7.Jinsi ya kulinda mawasiliano yako na Mungu yasikatike.

Tutaendelea kujifunza  hatua nyingine wakati ujao,endelea kutufuatilia katika mtandao wetu wa twitter,facebook na tuvoti yetu ya   www.mgmtministry.org

Mwisho, tuwasiliane ili uweze kupata kitabu kinachoitwa “Loliondo kwa Babu” kwa shs  elfu 10 tu kwa kukutumia  kwa posta ni shs elf 12,000. Tuwasiliane kwa kuniandikia kwa e-mail:mgmtza@hotmail.com simu no:+255-0784-517603,0759-357561 ili ukipate kwani ukikipata utakuwa umepata mambo yafuatayo:

-Jinsi huduma ya “Babu wa Loliondo” ilivyoanza,

-Watu waliokunywa kikombe cha babu walipona au la

– Jinsi Steven Kanumba na Babu wa Loliondo walivyohusiana

-Jinsi roho zidanganyazo zinavyofanya kazi katika kipindi hiki cha siku za mwisho

-Babu yuko wapi na anafanya nini sasa? Na mengine mwengi.

Kama uko nje ya nchi, ni vema uniandikie ili nijue nitakutumiaje kama utakihitaji au utavihitaji kwa wingi.

 

Karibu sana na ubarikiwe,

Mwinjilisti  Moses E. Malugu.

Mkurugenzi  na  Mwanzilishi wa huduma ya MGMT.

4 Responses to Somo la Maombi

Leave a Reply

Jiunge

Weka barua pepe yako kupokea Ujumbe wa Neno la Mungu

Aina za Mada
Mada kwa Mwezi